Home » » Waziri amkana Mkapa Arumeru

Waziri amkana Mkapa Arumeru

Written By Koka Albert on Wednesday, March 28, 2012 | 4:33 AM


ASEMA HAKUNA TATIZO LA ARDHI, WARAKA WASAMBAZWA KUMPINGA SIOIWaandishi Wetu, Arumeru
NAIBU Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Goodlucky Ole Medeye amewatetea walowezi wanaomiliki maeneo makubwa ya ardhi katika Jimbo la Arumeru Mashariki kwamba wanamiliki mashamba hayo kwa mujibu wa sheria.
Kauli ya Ole Medeye ambaye alikuwa akimnadi mgombea wa CCM, Sioi Sumari katika kampeni za uchaguzi mdogo wa jimbo hilo inapingana na ile iliyotolewa na Rais Mstaafu, Benjamin Mkapa alipokuwa akizindua kampeni za CCM, Machi 12 mwaka huu mjini Usa River.
Kadhalika, kauli hiyo inapingana na kauli zote za makada wa CCM na vyama vya upinzani akiwamo mgombea wa CCM Sioi ambao wanakiri kuwapo kwa matatizo makubwa ya ardhi Arumeru, huku wakiahidi kuyashughulikia.
Mkapa akizungumzia matatizo ya ardhi siku ya uzinduzi huo, kwanza alikanusha kuwa na ubia na walowezi hao lakini akakiri kuwapo kwa matatizo hayo huku akiahidi kwamba atafikisha suala hilo kwa Rais Jakaya Kikwete ili alipatie utatuzi.
Mkapa alikiri kupokea taarifa za kuwapo kwa migogoro mikubwa ya ardhi inayosababishwa na baadhi ya wawekezaji kuhodhi maeneo makubwa na kusema kwamba kero hiyo iko katika hatua mbalimbali za utatuzi wake.

“Yapo matatizo kadha wa kadha, wapo wawekezaji ambao wamehodhi maeneo makubwa wakati hawayatumii, wapo ambao wamechukua maeneo na kubadilisha matumizi yake na wapo ambao wamekiuka sheria za uendeshaji wa maeneo waliyopewa,” alisema Mkapa.
Alisema suala hilo atalifikisha kwa Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete na kumshauri achukue hatua kwa kuwawajibisha watendaji wa serikali ambao wameshindwa kuwajibika na kuchukua hatua za kisheria kwa wawekezaji waliokiuka masharti.
Lakini jana, Ole Medeye alisema mashamba yote 13 yanayotajwa yanamilikiwa kihalali na kwamba ikiwa kuna tatizo lolote basi wizara yake itafuatilia ili kuchukua hatua.
“Masuala ya umiliki wa ardhi yanasimamiwa na sheria za nchi, kwa hiyo wawekezaji hawa wanaotajwa, wanamiliki maeneo yao kwa mujibu wa sheria. Sasa kama kuna maeneo hayajaendelezwa basi hilo ni suala la kuona jinsi ya kuchukua hatua,” alisema Medeye katika mkutano wa kumnadi Sioi uliofanyika katika Kijiji cha Sing’isi.
Share this article :

Post a Comment

KARIBU KATIKA WEBSITE YA KIJANJA, KUPATA HABARI MBALIMBALI ZA NDANI NA NJE YA NCHI. PIA UTAPATA MAMBO YA ACADEMIC. KARIBU SANA
 
Support : Creating Website | Johny Template | Mas Template
Copyright © 2011. GetInformedTz - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Mas Template
Proudly powered by Blogger