Home » » Waarabu washtukia janja ya Simba

Waarabu washtukia janja ya Simba

Written By Koka Albert on Friday, March 16, 2012 | 12:02 AM

WAARABU wameishtukia mbinu ya Simba ya kupanga mechi kuchezwa na jua kali la saa 9:30 alasiri, huku wakitenga Euros 450 milioni kwa ajili ya michezo hiyo ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Kwa mujibu wa taarifa ya ES Setif inasema mechi hiyo inatarajiwa kuchezwa Machi 25 saa 9:30 Alasiri sawa na saa 7:30 mchana nchini Algeria.

Kutokana na uamuzi huo wa Simba, uongozi wa Setif 'Mwewe Mweusi' umepanga kutua nchini siku nne kabla ya mechi na kuandaa bajeti ya  jumla ya euros 450 milioni kwa ajili ya michezo hiyo miwili.

Katika mchezo wa kwanza wamepanga kutumia euros 270 milioni kwa ajili ya gharama za safari hiyo na euros 45 milioni zitatumika kwa matumizi maalumu.

Msafara wa timu hiyo utakuwa na watu 31. Watu 25 watagharamiwa na Simba na wengine sita watalipiwa na  ES Setif. Fedha zitakazobaki kati ya hizo euros 450 milioni zitagharamia mchezo wa marudiano utakaofanyika nyumbani kwa Setif.

Katika kuhakikisha wanakabiliana na hali hewa ya joto kali, Setif wamepanga kutua Dar es Salaam siku ya Jumatano Machi 21, saa 12 asubuhi wakitokea Misri ili kupata muda wa siku nne za mazoezi na kuzoea hali ya hewa ya joto ambayo ni tofauti na kwao hivi sasa ambako ni baridi.

Baadhi ya nyota wa Setif wamesema hiyo itakuwa ni safari ndefu na kuchosha wakitumia zaidi ya saa 13 angani.

Safari yao itaanza Jumanne saa 7 mchana, Machi 20, kuelekea Cairo ambako watafika saa 11:45 jioni na wanategemewa kukaa Misri kwa zaidi ya saa saba kabla ya kupanda ndege kuelekea Dar es Salaam ambapo watafika saa 12 asubuhi.

Katika kuthibitisha kwamba wanaifuatilia Simba kwa karibu Setif wanafahamu kwamba wapinzani wao wanaongoza Ligi Kuu Tanzania kwa pointi 44 na watapumzika kwa wiki moja kabla ya mchezo huo.

Pia, ES Setif wamewapeleka wachezaji na viongozi watakaokuwa kwenye msafara huo kupata chanjo ya magonjwa katika taasisi ya Pasteur.

Aina hiyo ya chanjo imekuwa ni jambo la kawaida kufanywa katika miaka ya hivi karibu kwa timu za nchi hiyo zinapocheza mechi zake Kusini mwa Jangwa la Sahara.

Kocha Alain Geiger na wachezaji Aoudia na Bengoreine mwaka 2010 walipokuwa na klabu ya JSK walifanya safari zao katika nchi nne za Gambia, Angola, Congo na Nigeria bila ya kuchukua tahadhali hiyo.

Kutokana na rekodi hiyo uongozi wa Setif umewataka kuhakikisha wapewe chanjo hiyo haraka.

Akiuzungumzia mchezo huo kocha Geiger alisema wachezaji wake wanatakiwa kubadilika zaidi kama kweli wanataka kushinda.

"Tunatakiwa kucheza kwa kiwango chetu kila tunachokionyesha katika ligi ili kufanikisha ndoto yetu ya kutafuta ubingwa wa michuano hii."

"Tunapaswa kushambulia kwa kasi na kujilinda vizuri zaidi, katika mechi iliyopita dhidi ya JS Saoura tulifanya makosa na kuruhusu mabao mawili sio kitu kizuri hivyo hivi sasa nafanyia kazi jambo hilo."

Kocha huyo pia ameutaka uongozi Setif kuhakikisha wanafanikisha kupatikana kwa wakati hati ya kusafiria kwa kiungo wake Amir Karaoui.

"Karaoui ni lazima awepo kwenye kikosi kitachokwenda Tanzania ni vizuri suala lake la hati ya kusafiria likashughurikiwa kwa haraka naye pia akapate chanjo,"alisema kocha Geiger.
Share this article :

Post a Comment

KARIBU KATIKA WEBSITE YA KIJANJA, KUPATA HABARI MBALIMBALI ZA NDANI NA NJE YA NCHI. PIA UTAPATA MAMBO YA ACADEMIC. KARIBU SANA
 
Support : Creating Website | Johny Template | Mas Template
Copyright © 2011. GetInformedTz - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Mas Template
Proudly powered by Blogger