Home » » Serikali kufunga shule na vyuo

Serikali kufunga shule na vyuo

Written By Koka Albert on Monday, March 26, 2012 | 4:57 AM

SERIKALI imesema, itafunga shule na vyuo vyote ambavyo havijasajiliwa na ambavyo havijakidhi vigezo na viwango vya kutoa elimu  nchini ili kulinda hadhi ya elimu ya Tanzania iliyovamiwa na soko holela.
Hayo yalibainishwa na Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo Stadi nchini, Philiph Mulugo wakati wa akihitimisha kilele cha maadhimisho ya Wiki ya Mamlaka Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (Veta), yaliyofanyika kitaifa kwenye viwanja vya Tangamano jijini Tanga.
Akizungumza kwa ukali, Mulugo alisema  sekta ya elimu haiwezi kuachwa hivi hivi kama haina mwenyewe, haiwezekani elimu ikaendeshwa kiholela.
Alisema haiwezekani mwanafunzi wa darasa la saba anajiunga na shule ya sekondari huku hajui kusoma na kuandika.
“Siku hizi kuna matangazo mengi ya shule na vyuo kwenye vyombo vya habari ambavyo havijasajiliwa, hivyo nimeagiza Veta kufanya ukaguzi na kuvibaini vyuo holela na kuvifunga ili kulinda hadhi ya elimu yetu,”alisema.
Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Veta, Profesa Idrissa Mshoro  aliwataka Watanzania kubadili mtazamo kuhusu vyuo vya Veta, wakidhani ni kwa ajili ya wale waliofeli darasa la saba au kidato cha nne.
Alisema Veta sasa inatoa mafunzo kwa wote na kuna fani mpya ambazo zinahitaji wahitimu waliofaulu vizuri.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Veta, Zebadia Moshi aliwataka wadau wa elimu kujenga zaidi vyuo vya ufundi na kwa kuwa ni suluhisho pekee la tatizo la ajira kwa vijana.
Alisema vijana wakipatiwa elimu ya ufundi, na kupewa vifaa,  wataweza kujiajiri wenyewe baada ya kumaliza mafunzo ya Veta.

Wadau mbalimbali wa Veta, waliipongeza taasisi hiyo kwa kuandaa maonyesho hayo kitaifa, lakini waliitaka Veta ijitangaze zaidi kwa kufanya maonyesho ya shughuli zake mara kwa mara katika maeneo yao na sio kusubiri mpaka muda wa maonyesho.

Maadhimisho hayo ya  wiki moja, yamehusisha maonyesho ya kazi mbalimbali zinazofanywa na vyuo vya Veta nchini na kuhusisha wajasiriamali wadogo wadogo waliowezeshwa na taasisi hiyo.

Share this article :

Post a Comment

KARIBU KATIKA WEBSITE YA KIJANJA, KUPATA HABARI MBALIMBALI ZA NDANI NA NJE YA NCHI. PIA UTAPATA MAMBO YA ACADEMIC. KARIBU SANA
 
Support : Creating Website | Johny Template | Mas Template
Copyright © 2011. GetInformedTz - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Mas Template
Proudly powered by Blogger