Home » » JK: Polisi aliyetinga disko na SMG afutwe

JK: Polisi aliyetinga disko na SMG afutwe

Written By Koka Albert on Wednesday, March 7, 2012 | 6:01 AM

Rehema Matowo, Moshi
 Rais Jakaya Kikwete amesema matendo ya utovu wa nidhamu likiwamo la askari kuingia disko na bunduki,yasivumiliwe kwa sababu ni ya hatari na yanaweza kuondoa uhai wa watu wasiokuwa na hatia.Akizungumza katika mkutano wa kuboresha jeshi la polisi, uliofanyika jana katika chuo cha Polisi Moshi na kuhudhuriwa na maofisa waandamizi, Rais Kikwete aliwataka viongozi hao kusimamia nidhamu ya askari wake.

Alisema askari asiyekuwa na nidhamu ndani ya jeshi hilo hafai kuwapo bali ni mamluki aliyeingia ndani ya jeshi.
 Alisema sifa ya kwanza ya polisi ni kuwa na nidhamu na kwamba anapokosa hafai kuwa polisi.Kikwete alisema taarifa ya askari kuingia disko na bunduki aliisoma kwenye gazeti hili na kwamba kitendo hicho kimeonyesha dhahiri kuwa wapo askari ambao hawana nidhamu.

“Nimesoma kwenye gazeti, askari hapa Moshi ameacha lindo na kuingia disko na bunduki huyu mtasema ni askari wenu kweli, amelitia aibu jeshi la polisi na hafai kuwa polisi, wachunguzeni askari wenu mtabaini ni walevi, wala rushwa na muwaonye mara moja akirudia watoeni maana hawawafai,”alisema.

Rais Kikwete aliutaka uongozi wa polisi kuangalia upya utaratibu wa vijana wanaoomba nafasi za kujiunga na jeshi hilo kwani itafika mahali jeshi hilo litaonekana ni la wahuni na sio la ulinzi wa raia na mali zao.

Aliwataka kuwa na utaratibu wa ndani wa kuangalia tabia za askari wao ili wajue tabia zao na kuzirekebisha kabla hazijaleta madhara kwa wananchi .

“Mimi nimepata malalamiko mengi tu kwa wananchi wapo wanaolala baa ,walevi,wahuni,wala rushwa,wapo wanaoshirikiana na majambazi, wachunguzeni mkiwabaini waonyeni kwa mara ya kwanza wakirudia watoeni wapo vijana waaadilifu wanatafuta nafasi hizo hawajazipata, wanaochezea watoeni,”alisisitiza.

Alisema kwa kufanya hivyo itawasaidia kujenga imani kwa wananchi na kuondokana na lawama zinazotolewa kwa jeshi hilo mara kwa mara. Alitaka jeshi hilo kuweka utaratibu utakaowasaidia wananchi kutoa malalamiko yao kwa uhuru na bila hofu.

Alitaka jeshi hilo kutoa mafunzo ya ueledi kwa askari wake kwani mafunzo ya ueledi ni msingi wa jeshi hilo. "Kuvaa magwanda sio kuthibitisha kuwa huyu ni askari anayefaa,"alisema.

Alisema magwanda na vifaa vya kisasa havitamjenga askari kama hana mafunzo ya ueledi ambayo yatampa mbinu za kukabiliana na uhalifu katika kipindi hiki wahalifu wamekuwa wakitumia mbinu za sayansi na teknolojia kufanya maovu.
Share this article :

Post a Comment

KARIBU KATIKA WEBSITE YA KIJANJA, KUPATA HABARI MBALIMBALI ZA NDANI NA NJE YA NCHI. PIA UTAPATA MAMBO YA ACADEMIC. KARIBU SANA
 
Support : Creating Website | Johny Template | Mas Template
Copyright © 2011. GetInformedTz - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Mas Template
Proudly powered by Blogger