Home » » Abiria zaidi ya 400 wa MV Maendeleo wakwama Kisiwani Pemba

Abiria zaidi ya 400 wa MV Maendeleo wakwama Kisiwani Pemba

Written By Koka Albert on Thursday, March 1, 2012 | 11:17 PM

ABIRIA zaidi 400 wamekwama baada ya meli ya Mv Maendeleo iliyokuwa inasafiri kutoka Unguja kwenda Pemba kushindwa kushusha abiria katika bandari ya Mkoani, Kisiwani Pemba hapo jana.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa watu waliokuwa ndani ya meli hiyo waliozungumza na gazeti hili kwa njia ya simu walisema meli hiyo ilipoteza mwelekeo na kuingia sehemu ambayo ilipelekea kukwama.

Meli hiyo inayomilikiwa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), ilipoteza mwelekeo wakati inajiandaa kufunga nanga na kusimama kwenye kina kifupi cha maji kilometa kama 100 kutoka bandari ya Mkoani ambayo hutumika kushusha abiria.

Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Usafiri wa Baharini Zanzibar (ZMA), Abdallah Hussein Kombo alithibitisha kukwama kwa meli hiyo kwenye eneo lenye kina kifupi cha maji ambapo alisema tukio hilo halikusababisha madhara yoyote kwa abiria waliokuwamo ndani ya meli hiyo wala athari kwa meli yenyewe.

Alisema kazi ya kuwaondoa abiria kwenye meli hiyo na kuwafikisha nchi kavu kisiwani Pemba ilifanyika baada ya serikali kupata taarifa hiyo na  kuwaingiza katika meli nyengine ya Mv Jitihada na meli za Jeshi la Wanamaji Zanzibar (KMKM) ambazo zilifanya kazi kubwa ya kuwafikisha bandarini.

“Taarifa zilizopo ni kuwa abiria wote zaidi ya 400 wako salama, na hakuna athari zilizopatikana katika tukio hilo ” alisema Kaimu Mkurugenzi huyo.

Wakizungumza kwa njia ya simu baadhi ya abiria waliokwama ndani ya meli hiyo walisema walikuwa na hofu kubwa kutokana na kuwa wahusika wa meli hiyo hawajasema lolote kwa abiria wao jambo lilizusha hofu miongoni mwa abiria.

Aidha wananchi waliokuwapo ndani ya meli hiyo wamelalamikia mamlaka zinazohusika kushindwa kuchukua hatua za dharura wakati inapotokea tatizo katika meli hizo na pia kulalamikia hali mbaya iliyokuwa ndani ya meli hiyo.

 Meli ya Mv Maendeleo iliondoka juzi usiku majira ya saa 3 na ilitarajiwa kufika saa 11:30 asubuhi na kushusha abiria lakini abiria hao waliokuwamo ndani ya meli hiyo wamekaa zaidi ya saa 6 ndani ya meli hiyo kabla ya meli za Mv. Jitihada na boti za KMKM kutakiwa kwenda kuwashusha abiria hao na kuwapeleka katika bandari ya Mkoani.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka vyanzo mbali mbali zinasema kwamba meli hiyo aidha ilipoteza mwelekeo kutokana na upepo mkali uliovuma jana na kusababisha maboya kusogea mbele na kuchukuliwa na upepo huo au nahodha alizidiwa na usingizi na kuipeleka meli pasipo pahala pake ambapo ilipanda juu ya mchanga.

Share this article :

Post a Comment

KARIBU KATIKA WEBSITE YA KIJANJA, KUPATA HABARI MBALIMBALI ZA NDANI NA NJE YA NCHI. PIA UTAPATA MAMBO YA ACADEMIC. KARIBU SANA
 
Support : Creating Website | Johny Template | Mas Template
Copyright © 2011. GetInformedTz - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Mas Template
Proudly powered by Blogger