Home » » Wananchi wavunja kituo cha polisi, wachoma nyumba za askari

Wananchi wavunja kituo cha polisi, wachoma nyumba za askari

Written By Koka Albert on Sunday, March 4, 2012 | 9:54 PM

WANANCHI wilayani Chunya, Mbeya  wamevamia Kituo cha Polisi Lupa Tinga Tinga na kukivunja kisha kuharibu mifumo ya mawasiliano huku wakichoma moto nyumba tatu, mbili kati ya hizo zikiwa za askari polisi na moja ya raia.

Tukio hilo lilifanyika kufuatia madai ya polisi kumpiga hadi kumuua, mwanafunzi wa kidato cha pili katika Shule ya Sekondari Lupa Tingatinga, Said Msabaha aliyekuwa akituhumiwa kuiba simu ya mkononi.

Moja wa wananchi aliyeshuhudia tukio hilo lilitokea juzi majira ya saa 10:00 jioni, aliliambia gazeti hili kuwa wananchi hao walianza vurugu hizo ikiwa ni pamoja na kuchoma matairi barabarani, sambamba na kuvunja kituo hicho cha polisi, ambapo inadaiwa mahabusu waliokuwepo walitoroka, wakiwemo wasomali.


"Wananchi hao pia walivamia nyumba walizopanga askari wengine, wakaingia ndani na kutoa vyombo na mali nyingine nje na kuliteketeza kwa moto duka la vinywaji la askari polisi mmoja," alisema mwananchi huyo.


Akizungumzia tukio hilo, Mwenyekiti  wa Kijiji cha Lupa Tingatinga, William Mbawala, alisema kabla ya kifo cha mwanafunzi huyo, alizungumza naye nakwamba alimwambia, yeye (wanafunzi huyo) na wenzake watatu walipigwa na polisi, wakidaiwa kuiba simu.

Habari kutoka ndani ya kikao cha pamoja cha usuluhishi kati ya Jeshi la Polisi na wananchi hao zinadai kuwa mbali na tukio hilo, wananchi hao walipa nafasi ya kueleza kero mbalimbali wanazopata kutoka kwa polisi wa kituo hicho.

Kikao hicho kilikuwa chini ya Ofisa Upelelezi Mkoa (RCO), Elias Mwita pamoja na madiwani na wenyeviti wa vijiji vya Ivuma na Lupa.


Wananchi walimwomba RCO kuwahamisha askari wote wa kituo hicho kwa madai kwamba wamekithiri kwa vitendo vya rushwa na wamekuwa wakiwabambika kesi na kuwanyanyasa  bila sababu.
Share this article :

Post a Comment

KARIBU KATIKA WEBSITE YA KIJANJA, KUPATA HABARI MBALIMBALI ZA NDANI NA NJE YA NCHI. PIA UTAPATA MAMBO YA ACADEMIC. KARIBU SANA
 
Support : Creating Website | Johny Template | Mas Template
Copyright © 2011. GetInformedTz - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Mas Template
Proudly powered by Blogger