Home » » Magufuli atangaza operesheni safisha Dar

Magufuli atangaza operesheni safisha Dar

Written By Koka Albert on Monday, March 5, 2012 | 10:40 PM


Joseph Zablon
WAZIRI wa Ujenzi, Dk John Magufuli amempa siku tano Meneja wa Wakala wa Barabara (Tanroads), Mkoa wa Dar es Salaam awe amewaondoa katika hifadhi za barabara watu wanaoendesha shughuli zao katika maeneo hayo kinyume cha sheria.

Amri hiyo ya Dk Magufuli inaagiza kuondolewa kwenye maeneo hayo wachuuzi wa bidhaa mbalimbali pamoja na magari yanayoegeshwa sehemu hizo kiasi cha kuayafanya kuwa gereji bubu.

Agizo hilo la Dk Maguguli limekuja kipindi ambacho Jiji la Dares Salaam ambalo ni kitovu cha shughuli za kiuchumi na biashara nchini, likiwa linakabiliwa na tatizo la msongamano wa magari, ambalo pamoja na mambo mengine, linatokana na ukiukwaji wa sheria mbalimbali zikiwamo za barabarani.

Jana, akizungumza wakati wa uzinduzi wa stendi mpya ya mabasi Mbezi Mwisho jijini Dar es Salaam, Dk Magufuli alisema hakuna sababu ya watu hao kubaki katika hifadhi za barabara wakati sheria zipo na kusisitiza, "Hata kama mkikuta milingoti ya bendera ya CCM vunjeni."

Dk Magufuli alisema, Sheria ya Barabara ya mwaka 1987 inasema wazi kuwa mtu ambaye atakutwa anafanya biashara, kuegesha gari, kumwaga mafuta au uvamizi mwingine wa namna yoyote katika hifadhi ya barabara, adhabu yake ni faini ya Sh1 Milioni.

Alimwagiza meneja huyo kuwa Tanroads haipo kisiasa na wao wapo kusimamia sheria na sio vingine. "Mpo kusimamia sheria, acheni kupiga siasa," alisisitiza.

Huku akishangiliwa na umati wa watu waliohudhuria uzinduzi huo, Dk Magufuli alisema ni lazima ndani ya siku hizo tano, wachuuzi na waliovamia hifadhi za barabara kuondolewa na kusisitiza kuwa sheria haina chama, iwe Chadema, CCM ama kingine chochote.

"Mnyika (John ambaye ni Mbunge wa Ubungo) kawaambie wenzako wa CUF, UPDP na vyama vingine kuwa sheria haina mswalie mtume," alisisitiza Dk Magufuli, huku akiwaonya watendaji wa manispaa ambao wameshindwa kuchukua hatua dhidi ya wanaovunja sheria.

Dk Magufuli alitoa mfano wa wafanyabiashara wa eneo la Tegeta jijini Dar es Salaam ambao wamekuwa wakikwaza ujenzi wa barabara ya Bagamoyo kutokana na kupanga bidhaa zao barabarani.

''Ukienda Tegeta watu wamepanga biashara barabarani, Mkuu wa Mkoa upo, Mbunge yupo, Mkuu wa Polisi Wilaya (OCD) yupo, diwani yupo, mkuu wa wilaya naye pia na wote hao wanaangalia tu, ndio Tanzania hiyo?," alihoji na kusisitiza kuwa ifike sehemu sheria iachwe ifanye kazi.

Alisema kutokana na hali hiyo, biashara ya namna yoyote haitaruhusiwa katika stendi mpya ya Mbezi Mwisho na hakuna tozo yeyote kwa daladala na mabasi ya abiria ambayo yataitumia stendi hiyo.

Foleni Dar
Katika hatua nyingine, Dk Magufuli alieleza kuwapo kwa miradi mitano inayotekelezwa ili kupunguza msongamano katika Jiji la Dar es Salaam.

Alisema Sh350 milioni zimepatikana mpaka sasa kwa ajili ya ununuzi wa kivuko ambacho kitasafirisha abiria kutoka Bagamoyo hadi jijini Dar es Salaam kwa kutumia gati saba zitakazowekwa katika maeneo tofauti hadi eneo la Feri.

"Tunakusanya pesa kwa ajili ya Kivuko hicho na hadi sasa zimepatikana Sh 350milioni na sio lazima kila ajaye mjini kutoka eneo ambako bahari inapita apande daladala," alisema Magufuli.
Share this article :

Post a Comment

KARIBU KATIKA WEBSITE YA KIJANJA, KUPATA HABARI MBALIMBALI ZA NDANI NA NJE YA NCHI. PIA UTAPATA MAMBO YA ACADEMIC. KARIBU SANA
 
Support : Creating Website | Johny Template | Mas Template
Copyright © 2011. GetInformedTz - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Mas Template
Proudly powered by Blogger