Home » » Stars imedorora, inakera, haina morali

Stars imedorora, inakera, haina morali

Written By Koka Albert on Saturday, March 3, 2012 | 12:23 AM

TAIFA Stars imedorora, inakera, haina morali. Jumatano jioni ilishindwa kupata ushindi mnono dhidi ya Msumbiji katika mechi ya kufuzu kwenda hatua ya makundi kwa michuano ya AFCON mwakani.

John Boko alijigeuza Torres
Mara ya mwisho nilimtetea John Boko katika pambano dhidi ya DRC Congo kwamba timu haikumlisha mipira. Alipata wakati mgumu kweli kweli. Lakini katika pambano dhidi ya Msumbiji alilishwa vizuri mipira na timu ilimsogelea lakini bado akaonekana nyanya katika kumalizia.

Boko alikuwa na siku mbaya, lakini pia siku mbaya hii alitengenezewa zaidi na mashabiki mara baada ya kukosa bao la wazi katika dakika za mwanzo. Kuanzia hapo mashabiki wakamzomea na uwezo wake wa kujiamini ukatokomea kusikojulikana. Alifanana sana na kivuli cha mshambuliaji wa Chelsea, Fernando Torres.

Sub mbovu za Jan Poulsen
Kwa nini Nizar Khalfan alitolewa wakati wa mapumziko? Jibu analo kocha Jan Poulsen, lakini mara baada ya kuondoka kwa Nizar, Stars ilishindwa kumiliki mpira zaidi pale katikati. Aliyeingia, Mrisho Ngassa, ni mkimbizaji zaidi kuliko Nizar

Hata kuondoka kwa Vincent Barnabas uwanjani kulikuwa tatizo. Vincent Barnabas alikuwa mpishi wa bao la Stars ingawa baadaye alikosa mabao mawili ya wazi. Lakini walau yeye alikuwa mbunifu uwanjani kuliko Hussein Javu.

Kwa nini Poulsen anang�ang�ania kumchezesha Javu pembeni? Javu ni mshambuliaji mwenye madhara zaidi akiwa katikati. Kumchezesha pembeni ni kumpa mzigo mzito usio na maana.
Mechi dhidi ya Congo, Javu alianza na hakuonyesha maajabu yoyote kwa kucheza pembeni. Mechi hii pia hadithi ilikuwa ile ile baada ya kuingia uwanjani.

Domingues ni yule yule
Oktoba 4, 2006 Stars ilicheza na Msumbiji mechi ya kwanza kabisa katika zama mpya za Rais Jakaya Mrisho Kikwete pale Uwanja wa Machava, Maputo.

Pambano lilikwisha kwa suluhu, lakini Elias Pelembe, maarufu kama Domingues, alisababisha wachezaji wa Stars walale na viatu baada ya mechi.

Siku ile pale Machava alikuwa amevaa jezi namba 7, wakati tuliporudiana nao Dar es Salaam alivaa jezi namba 7 na Jumatano alivaa jezi namba 10. Huyu jamaa ni msumbufu na anachezea mpira balaa.

Na yeye na wenzake wawili pale mbele ndio waliondoa uwiano wa timu yetu ya taifa katika mashambulizi na kujihami. Poulsen hakujua akazane katika jambo gani. Na ndiyo maana hata bao ambalo Stars walifungwa lilikuwa moja kati ya mabao rahisi zaidi waliyowahi kufungwa miaka ya karibuni
Share this article :

Post a Comment

KARIBU KATIKA WEBSITE YA KIJANJA, KUPATA HABARI MBALIMBALI ZA NDANI NA NJE YA NCHI. PIA UTAPATA MAMBO YA ACADEMIC. KARIBU SANA
 
Support : Creating Website | Johny Template | Mas Template
Copyright © 2011. GetInformedTz - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Mas Template
Proudly powered by Blogger