Home » » Yanga watishiwa vifaru vya jeshi

Yanga watishiwa vifaru vya jeshi

Written By Koka Albert on Saturday, March 3, 2012 | 12:20 AM

MICHAEL MOMBURI, CAIRO
PATA picha hasa wewe mkazi wa jiji la Dar es Salaam. Unakwenda pale Ubungo kwenye mataa unakuta kifaru cha kivita kimeegeshwa kikifanya doria badala ya magari la Polisi au askari wa pikipiki.

Ndivyo wanavyoshangaa wachezaji wa Yanga hapa jijini Cairo kwani mitaani ni vifaru tu ambavyo vinafanya doria.

Misri, ambayo ipo chini ya uongozi wa kijeshi kwa sasa baada ya kuondolewa madarakani Rais wake, Hosni Mubarak, leo Jumamosi itaiweka Yanga chini ya ulinzi mkali wa kila aina ambao vijana hao wa Jangwani hawajawahi kukutana nao na pengine hawawezi kukutana nao tena maisha yao yote.

Yanga inarudiana na Zamalek kwenye mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwenye Uwanja wa Chuo cha Jeshi la Misri ulioko kilometa kadhaa nje ya mji karibu na eneo la Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Cairo.

Katika mechi ya awali timu hizo zilitoka sare ya bao 1-1, jambo ambalo linailazimu Yanga kusaka sare ya mabao 2-2 hapa au ushindi ili kusonga mbele ingawa wachezaji wameonekana kuwa na uchangamfu na kujiamini hasa mastraika Jerry Tegete, Hamis Kiiza na Kenneth Asamoah.

Wengine, hususani wale ambao hawana uhakika kwenye kikosi cha kwanza au waliokwishazoea benchi, wameonekana kuwa na mtingo wa mawazo tangu wakiwa kwenye ndege na hata baada ya kuwasili mjini kana kwamba wanaishi ilimradi ingawa muda fulani hulazimisha kujichekesha.

UWANJA WA JESHI
Uwanja huo wa Jeshi unaogopwa na mashabiki wa hapa kutokana na ulinzi mkali wa wanajeshi ambao huwa hawapendi utani wala vurugu na wakazi wa hapa wanasema hata kama kuna mechi ya ligi ya ndani inachezwa kwenye uwanja huo, mashabiki huwa ni wachache kwani hukosa uhuru kama viwanja vingine.

Ofisa mmoja wa kijeshi akizungumza kwa msaada wa tafsiri ya Mtanzania mmoja anayeishi jijini hapa, alisema; Kule si Tahrir Square (sehemu kuu ya makutano katikati ya jiji iliyozoeleka) ni kitu kingine kabisa, ndiyo maana hata mechi za ligi wanakwenda wachache, tena kwa nidhamu kubwa.

Uwanja huo utakuwa na utitiri wa askari wenye silaha kali za kivita kuzunguka mitaa ya karibu, nje ya uwanja na ndani ya uwanja na hakutakuwa na mashabiki zaidi ya watendaji na viongozi wasiozidi 100 wa timu zote mbili.


Ingawa mashabiki wamekuwa na tabia za kufanya fujo nje ya mageti wanapozuiwa, lakini hawataweza kuiona Yanga kwa kuwa wengi wameingiwa na hofu kutokana na jinsi mambo yanavyoendeshwa kijeshi ambapo ukikutwa na kosa na kushikiliwa inakuchukua muda mrefu kurejea uraiani.
Yanga walitarajia kufanya mazoezi ya mwisho kwenye uwanja huo wa kijeshi jana Ijumaa usiku.

http://www.mwanaspoti.co.tz/wcreadnews.php?id=10787

Share this article :

Post a Comment

KARIBU KATIKA WEBSITE YA KIJANJA, KUPATA HABARI MBALIMBALI ZA NDANI NA NJE YA NCHI. PIA UTAPATA MAMBO YA ACADEMIC. KARIBU SANA
 
Support : Creating Website | Johny Template | Mas Template
Copyright © 2011. GetInformedTz - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Mas Template
Proudly powered by Blogger