Home » » Uamuzi wa kubadilisha wachezaji wanne leo

Uamuzi wa kubadilisha wachezaji wanne leo

Written By Koka Albert on Saturday, March 3, 2012 | 12:07 AM


LONDON, England
BODI ya kutunga sheria ya Shirikisho la Soka la Kimataifa Fifa inayoitwa IFAB leo itafanya uamuzi kuhusu kubadilisha mchezaji wa nne wakati wa muda wa dakika 30 za nyongeza.

Pia IFAB itafanya uamuzi kuhusu kutumia teknolojia kuangalia goli mpira unapovuka mstari na itafanya uamuzi juu ya uvaaji wa hijabu za kiislamu wakati wa mechi.

IFAB itafanya uamuzi huo katika mkutano wake wa 126 utakaofanyika huko Bagshot Magharibi ya Mji wa London, pia watajadili suala la adhabu tatu kwa mchezaji anayemzuia mwenzake anapokwenda kufunga ambazo ni kutolewa penati, kupewa kadi nyekundu na kutolewa uwanjani.

Suala lingine litakalojadiliwa ni kutumia rangi za kupuliza ambazo zilitumiwa katika Copa America mwaka jana, ambapo ilipotokea mipira ya adhabu mwamuzi alikuwa akipuliza kwenye majani baada ya kuhesabu hatua 10 za kuweka ukuta.

Katika mkutano wa leo, IFAB itasikiliza kwanza mapendekeo ya kubadilisha wachezaji wanne badala ya watatu katika dakika 120 wakati timu zitakapokuwa zimeenda muda wa nyongeza ili kuboresha mchezo wa soka na kupunguza wachezaji kuumia.

"Kikosi maalum cha Fifa 2014, Kamati ya utabibu ya Fifa na Kamati ya soka ya Fifa zinaunga mkono wazo hilo ili kuweza kupata burudani nzuri ya soka kiufundi ndani ya dakika 120 na kulinda usalama wa wachezaji,"ilisema taarifa ya Fifa.

IFAB pia itapitia majaribio ya kutumia mfumo wa waamuzi watano, ambapo kutakuwa na mwamuzi katika kila goli kwa ajili ya kumsaidia mwamuzi wa kati kufanya maamuzi.

Majaribio hayo ya kutumia waamuzi watano yalifanyika katika mashindano ya ubingwa wa Ulaya, pia waamuzi watano walitumiwa katika mechi za Ligi ya Mabingwa Ulaya na Europa Ligi msimu huu.

Katika mkutano huo pia Ali ambaye ni mtoto wa mfalme wa Jordan na mjumbe wa Kamati Kuu ya FIFA atawakilisha hoja ya kuondoa vikwazo kwa wachezaji soka wanawake kuvaa hijab.

Uvaaji wa hijabu kwa wachezaji soka ulipigwa marufuku miaka mitano iliyopita kwa sababu ya usalama.

Uamuzi utakaotolewa leo na IFAB utaanza kufanya kazi Julai 1 kabla ya kuanza kwa msimu mpya wa ligi za soka mbalimbali au katika mkutano wa leo wanaweza kuamua uamuzi watakaouchukua uanze kufanya kazi mara moja kama ilivyokuwa kwa vitambaa vya kuzuia baridi shingoni.

Share this article :

Post a Comment

KARIBU KATIKA WEBSITE YA KIJANJA, KUPATA HABARI MBALIMBALI ZA NDANI NA NJE YA NCHI. PIA UTAPATA MAMBO YA ACADEMIC. KARIBU SANA
 
Support : Creating Website | Johny Template | Mas Template
Copyright © 2011. GetInformedTz - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Mas Template
Proudly powered by Blogger